Meli za kijeshi za Urusi na China zathibitishwa kupita kusini magharibi mwa Japani

Wizara ya Ulinzi ya Japani inasema meli nne za Urusi na China zimethibitishwa kuwa zimepita kupitia mlango bahari kusini magharibi mwa Japani.

Wizara hiyo imesema Jeshi la Kujihami la Majini la Japani limezibainisha meli mbili za kijeshi za Urusi ikiwemo manowari na meli mbili za kijeshi za China ikiwemo ya kuharibu makombora.

Meli hizo zilithibitishwa kusafiri kuelekea mashariki takribani mwendo wa kilomita 40 nje ya Visiwa vya Kusagaki kwenye Mkoa wa Kagoshima juzi Alhamisi mchana.

Maafisa wanasema meli hizo zilipita kupitia Mlango Bahari wa Osumi uliopo kusini magharibi mwa Japani baadaye katika siku za Alhamisi na Ijumaa, na kusafiri kuelekea Bahari ya Pasifiki.

Hii ni mara ya tatu kwa meli za kijeshi za Urusi na China zilishuhudiwa zikisafiri kwa pamoja kupitia mlango bahari. Awali ziliwahi kushuhudiwa mwezi September mwaka 2022.

Wizara ya ulinzi ya Urusi ilitangaza juzi Alhamisi kwamba meli kutoka nchi hizo mbili zitafanya doria za pamoja. Wizara ya Ulinzi ya Japani inafuatilia kwa ukaribu shughuli zao.