Modi kuzuru Urusi kwa mazungumzo na Putin

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi anatazamiwa kuzuru Urusi wiki ijayo na kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Haya yanajiri huku Marekani na nchi zingine za Magharibi zikijaribu kuitenga Urusi kwa uvamizi wake dhidi ya Ukraine.

Wizara ya mambo ya nje ya India inasema Modi ataanza ziara ya siku mbili kuanzia Jumatatu na kufanya mazungumzo na Putin. Itakuwa ni ziara ya kwanza rasmi ya Modi nchini Urusi tangu uvamizi huo uanze.

India ni mshirika wa jadi wa Urusi katika maeneo kama vile ulinzi. Imekuwa mara kwa mara ikijiepusha na maazimio ya Umoja wa Mataifa ya kutaka vikosi vya Urusi viondolewe mara moja kutoka Ukraine, na kudumisha msimamo wa kutoegemea upande wowote. Lakini imekuwa ikiimarisha uhusiano wa kiuchumi na Urusi na kuongeza uagizaji wake wa mafuta ya Urusi.

Ikulu ya Urusi inasema mazungumzo hayo yatalenga katika kuendeleza uhusiano wa jadi wa kirafiki kati ya nchi hizo mbili, pamoja na masuala ya kikanda na kimataifa.