Chama cha Labour nchini Uingereza chapata ushindi mkubwa, Starmer kuwa Waziri Mkuu

Chama kikubwa cha upinzani nchini Uingereza cha Labour kimepata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu uliofanyika jana Alhamisi. Kimeshinda viti 326 kati ya 650 katika bunge la nchi hiyo.

Kiongozi wa chama cha Labour Keir Starmer anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Uingereza katika mabadiliko ya kwanza ya madaraka katika kipindi cha miaka 14 iliyopita.

Waziri Mkuu wa Uingereza Rishi Sunak leo Ijumaa amekiri kushindwa katika uchaguzi huo na kukiri kuwa chama cha upinzani cha Labour kimeibuka mshindi.

Sunak alisema, “Nimempigia simu Sir Keir Starmer kumpongeza kufuatia ushindi wake.” Aliongeza kuwa atawajibika kutokana na kushindwa na alisema kwamba “anaomba msamaha.”

Aliendelea, “Sasa nitaelekea mjini London ambako nitaongea mengi zaidi kuhusiana na matokeo ya leo usiku kabla ya kuacha kazi ya Waziri Mkuu ambayo nimeifanya kwa kujitolea zaidi.”