Kipimo cha Nikkei 225 chafikia rekodi ya juu zaidi

Kipimo cha wastani katika Soko la Hisa la Tokyo kimefikia rekodi ya juu kabisa katika muda wa biashara leo Ijumaa asubuhi. Kimevunja rekodi ya awali iliyowekwa takribani miezi mitatu iliyopita.

Kipimo cha Nikkei 225 kilipanda kwa muda mfupi hadi kiwango cha 41,100 mara tu baada ya soko hilo kufunguliwa. Wawekezaji walikimbilia kununua hisa za masuala yanayohusiana na semikondakta. Sarafu ya yeni imeendelea kuwa dhaifu katika soko la kubadilisha fedha za kigeni, na kupelekea matarajio makubwa ya kukua kwa biashara zinazohusiana na mauzo ya nje.