Japani kutangaza mpango wa msaada wa kutegua mabomu ya ardhini

Waziri wa Mambo ya Nje wa Japani Kamikawa Yoko anapanga kutoa tamko wakati wa ziara yake nchini Cambodia inayoanza leo Ijumaa. Hatua hizo zimejikita kwenye uzoefu wa miaka mingi wa Japani katika kutegua mabomu yaliyotegwa ardhini katika nchi hiyo iliyopo Kusini Mashariki mwa Asia.

Mpango wa Japani utajumuisha msaada mpana kama vile kuwafundisha watu namna ya kuepuka mabomu ya kutegwa ardhini na kuwasaidia waathiriwa wa milipuko.

Hatua mahususi ni pamoja na kutoa teknolojia za kutegua mabomu ya kutegwa ardhini zilizoendelezwa na kampuni za Japani kama vile vitambuzi vya mabomu hayo na vifaa vya kuyafukua na pia mfumo wa teknolojia ya akili mnemba, AI wa kutabiri maeneo yalikofukiwa mabomu ya ardhini.

Japani pia itatoa matbaa za kufanya chapa pande tatu, yaani 3D, kwa ajili ya kutengeneza viungo bandia.

Japani inapanga kuwaalika maafisa wa serikali ya Ukraine nchini Cambodia mwezi ujao kwa ajili ya mafunzo juu ya namna ya kutumia vifaa vya kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini.