Tahadhari za ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali zatolewa katika mikoa 21 nchini Japani

Wizara ya Mazingira na maafisa wa hali ya hewa nchini Japani leo Ijumaa wametoa tahadhari za ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali katika mikoa 21 huku halijoto za zaidi ya nyuzi 35 za Selisiasi zikitabiriwa katika maeneo mengi ya magharibi na mashariki mwa nchi hiyo.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa inasema halijoto zinatarajiwa kupanda kwa sababu mfumo wa mgandamizo mkubwa wa hewa juu ya bahari ya Pasifiki utafunika maeneo mengi ya magharibi na mashariki mwa Japani.

Mamlaka zinatoa wito kwa watu kuepuka kufanya mazoezi nje na ndani ya nyumba bila kuwasha viyoyozi.

Pia zinawashauri watu kuepukana na matembezi yasiyokuwa muhimu. Wanapaswa kunywa maji mara kwa mara hata ikiwa hawahisi kiu na kutosita kutumia viyoyozi nyumbani.