Biden akiri ‘hakufanya vizuri’ kwenye mdahalo

Rais wa Marekani Joe Biden amekiri kuwa “alikuwa na usiku mbaya,” “hakufanya vizuri” na “alifanya makosa” katika mdahalo uliorushwa kwenye runinga dhidi ya rais wa zamani Donald Trump wiki iliyopita. Lakini aliapa kusalia kwenye kinyang’anyiro cha urais.

Biden alizungumza katika mahojiano yaliyorushwa wakati wa kipindi cha redio jana Alhamisi. Kufanya vibaya katika mdahalo huo kwa Biden mwenye umri wa miaka 81 kumeibua mashaka juu ya umri wake, na kufanya mbunge mmoja wa chama cha Democrat kutaka kuondoa ushiriki wake katika kinyang’anyiro cha urais.

Biden alisema “hakuwa na mdahalo mzuri” wakati wa dakika zake 90 jukwaani. Lakini alitoa wito kwa wasikilizaji kutazama alichokitimiza katika kipindi cha miaka mitatu na nusu ya urais wake. Alisisitiza kuwa “aliongoza kufufuka kwa uchumi uliokaribia kuporomoka.”

Pia alitangaza nia yake ya kumshinda Trump na kushinda uchaguzi huo kama alivyofanya mwaka 2020.

Biden alitoa hotuba wakati wa tukio la kusherehekea Siku ya Uhuru Julai 4. Pia amepangiwa kuhojiwa katika kipindi cha runinga na kutoa hotuba katika jimbo lenye ushindani mkali katika siku chache zijazo.