China yapanga kudumisha hatua za ‘usalama’ miaka 15 baada ya vurugu katika eneo la Xinjiang

Inatimia miaka 15 leo Ijumaa tangu maandamano ya kuipinga serikali katika Eneo Linalojitawala la Xinjiang Uygur nchini China kuongezeka na kuwa yenye vurugu kubwa zilizosababisha vifo. China inaonekana kuwa tayari kudumisha kile inachokitaja kuwa ni hatua za usalama katika eneo la Xinjiang, licha ya kukabiliwa na shutuma za ukiukwaji wa haki za binadamu katika eneo hilo.

Watu wa kabila dogo la Uygur waliandamana katika mitaa ya mji wa Urumqi uliopo katikati ya eneo la Xinjiang Julai 5 mwaka 2009 kuipinga serikali ya China. Hata hivyo, maandamano hayo yaligeuka na kuwa yenye vurugu. Mamlaka zinasema takribani watu 200 walifariki.

Serikali baadaye iliimarisha juhudi zake za kukuza uchumi wa eneo la Xinjiang kwani hali ya kuvunjika moyo kutokana na tofauti kubwa ya kipato kati ya watu wa makabila ya Uygur na Han inaaminika kuwa moja ya vigezo vilivyosababisha maandamano hayo. Pato Ghafi la eneo hilo mwaka jana lilikuwa takribani mara 4.5 ya lile la mwaka 2009.

Mamlaka pia zilitekeleza hatua katika eneo la Xinjiang kuzuia kile zinachokiita kuwa ni mgawanyiko wa kikabila na ugaidi. Hatua hizo ni pamoja na kuwekwa kwa vizuizi kwa desturi za Kiislamu zinazofanywa na watu wa kabila la Uygur.

Kadhalika, China inasema kwamba imewapatia elimu na mafunzo watu wa kabila hilo katika vituo ili kuwaondolea mafundisho yenye itikadi kali.

Lakini China inakabiliwa na shutuma za kimataifa za kukiuka haki za binadamu katika eneo la Xinjiang kwa kisingizio cha mipango ya kukabiliana na ugaidi.
Idadi inayoongezeka ya watu wa kabila la Uygur pia wanalalamika kwamba wanafamilia wao wamewekwa kizuizini bila haki.

Maeneo kulikozuka vurugu yamegeuka kuwa vivutio vya watalii. Lakini hali ya usalama bado imeimarishwa zaidi katika maeneo hayo huku vifaru vikipelekwa.

China inaonekana kuwa na shauku ya kuelezea matokeo ya sera zake katika eneo la Xinjiang ikisema kuwa nchi hiyo haijashuhudia matukio yoyote ya kigaidi katika kipindi cha miaka saba iliyopita.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China amesisitiza kuwa eneo la Xinjiang kwa sasa linafurahia uthabiti wa kijamii, maendeleo ya kiuchumi, umoja wa kikabila, amani ya kidini na viwango vya maisha vinavyozidi kukua.