Joto kali laikumba mkoa wa Shizuoka na maeneo mengi kote nchini Japani

Joto kali limeshuhudiwa kote nchini Japani leo Alhamisi, nyuzi 39 za Selisiasi zilirekodiwa katika Jiji la Shizuoka. Watu wanashauriwa kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali.

Mamlaka ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini humo inasema mkandamizo mkubwa katika mfumo wa hewa kwenye bahari ya Pasifiki umeongeza viwango vya joto.

Joto lilifikia nyuzi 39.1 katika Jiji la Shizuoka, katikati ya Japani majira ya saa 6:40 mchana. Halijoto katikati mwa Tokyo ilifikia nyuzi 35 majira ya saa 6:31 mchana.

Mamlaka hiyo imetoa tahadhari ya ugonjwa wa kuzirai kutokana na joto kali katika mikoa 15.

Watu wanapaswa kuchukua tahadhari zaidi ili kuzuia ugonjwa huo kwa kutumia viyoyozi ipasavyo, kunywa maji mara kwa mara, kuepuka kufanya kazi na mazoezi ya nje kwa muda mrefu na kupumzika ipasavyo.