Maswali na Majibu: Tahadhari za kupanda Mlima Fuji (6)

(6) Kuepuka njia zilizojaa watu

NHK inajibu maswali kuhusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Mlima Fuji ambao ni mrefu zaidi nchini Japani, unavutia wapandaji mlima wengi raia wa kigeni kila mwaka. Lakini msongamano wa watu kupita kiasi na tabia za kutojali za wapandaji wengi zinasababisha matatizo mbalimbali, hivyo mamlaka zimetambulisha sheria mpya na hatua zingine. Katika kipengele hiki, tunaangazia juu ya kuepuka njia zilizojaa watu.

Njia za kupanda Mlima Fuji hujaa watu kupita kiasi kutokana na kufunguliwa kwa miezi miwili pekee kwa mwaka, kati ya Julai na Septemba. Tovuti rasmi kwa upandaji Mlima Fuji inasema njia ya jirani na kilele husheheni watu hususani mwishoni mwa juma na wakati wa msimu wa sikukuu za majira ya joto katikati ya mwezi Agosti, kati ya saa tisa usiku na mawio. Inasema msongamano wa watu unaweza kuwa mbaya sana hata wapandaji wakakumbwa na ugumu wa kusogea. Msongamano wa watu kwenye njia ya kupandia mlima wakati wa saa za usiku husababaisha mawe kuangukia wapandaji. Pia ni vigumu kuepuka mawe yanayoanguka kwa sababu ya msongamano na hiyo ni hatari sana.

Tovuti rasmi inawahamasisha wapandaji kuchagua siku na kuepuka saa zenye pilika nyingi. Pia inasema wapandaji wanaweza kushuhudia mawio kando ya njia, na si tu kwenye kilele cha mlima.

Wapandaji wanashauriwa kuangalia tovuti kubaini utabiri wa msongamano na maeneo ya kando ya njia ambapo huwa na kawaida ya kujaa watu. Tovuti hiyo pia inatoa taarifa juu ya maeneo ya kutazama mawio.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Julai 4, 2024.