Chama cha Labour chajipanga kushinda kwa kishindo katika uchaguzi nchini Uingereza

Watu kote nchini Uingereza wanaenda kupiga kura. Baada ya miaka 14, wanatarajiwa kuiondoa madarakani serikali yao inayoongozwa na chama cha Conservative.

Wagombea katika majimbo 650 leo Alhamisi wanawania kiti katika Bunge. Wale wa chama kitakachopata viti 326 watatawala kwa wingi wa kura za jumla.

Chama tawala cha Conservative kinaahidi kupunguza kodi, kulinda pensheni na kupunguza uhamiaji. Walipitisha mswada wa kuwapeleka nchini Rwanda waomba hifadhi wanaoingia Uingereza kinyume cha sheria.

Kiongozi wa Chama cha Labour Keir Starmer ameahidi kuleta uthabiti wa kiuchumi na kuboresha Huduma ya Afya ya Taifa, ikiwa ni pamoja na muda wa kusubiri matibabu. "Ikiwa unataka mabadiliko, unapaswa kuyapigia kura," aliwaambia wafuasi katika mkutano wa hadhara huko Worcestershire.

Makadirio ya mwisho ya YouGov yanaashiria kuwa chama cha Labour kitashinda kwa rekodi ya wingi wa viti 431 na chama cha Conservative kitapoteza theluthi mbili ya viti vyake, na kubaki na 102. Rishi Sunak anaweza hata kuwa waziri mkuu wa kwanza wa Uingereza kupoteza kiti chake mwenyewe.