Shirika la Ushirikiano la Shanghai laidhinisha rasmi uanachama wa Belarus

Shirika la Ushirikiano la Shanghai, SCO linaloendeshwa kwa pamoja na China na Urusi limeidhinisha rasmi uanachama wa Belarus ambayo ni mshirika wa Urusi.

Mkutano wa Baraza la Wakuu wa Nchi wanachama wa SCO ulifanyika jana Alhamisi katika mji mkuu wa Kazakhstan, Astana, kufuatia mazungumzo ya pande mbili siku iliyotangulia.

Rais wa Kazakhstan Kassym-Jomart Tokayev aliyeongoza mkutano huo alisema kwamba kwa kufanya kazi pamoja, nchi wanachama zimeifanya SCO kuwa moja ya mashirika ya kimataifa yenye ushawishi na mamlaka makubwa zaidi.

Aliongeza kusema kuwa maslahi ya dunia katika shirika hilo yanaongezeka kwa kasi.

Belarus iliidhinishwa rasmi kujiunga na shirika hilo kama mwanachama kamili wa kumi kwenye mkutano huo uliohudhuriwa na Rais wa nchi hiyo Alexander Lukashenko.

Urusi na China zinaonekana kutafuta kupanua shirika hilo kama mpangokazi wao wa kimataifa wa kukabiliana na mashirika yanayoongozwa na Marekani na Ulaya.

Mwaka jana, Iran ambayo inaunga mkono uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, ilijiunga rasmi na mpangokazi huo.