Maandamano makubwa dhidi ya chama cha mrengo mkali wa kulia yafanyika nchini Ufaransa

Maelfu ya waandamanaji wamekusanyika jijini Paris nchini Ufaransa kuwataka wapiga kura wasiruhusu ushindi wa chama cha mrengo mkali wa kulia katika duru ya pili ya uchaguzi wa bunge ulioitishwa haraka.

Chama cha mrengo mkali wa kulia cha National Rally na washirika wake kimeibuka kidedea katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa Bunge la Taifa, kikijinyakulia zaidi ya asilimia 30 za kura zote.

Duru ya pili ya uchaguzi itafanyika Jumapili ijayo katika maeneo ya uchaguzi yasiyopata washindi katika duru ya kwanza.

Vyama vya wafanyakazi, makundi ya haki za binadamu na waratibu wengine walikusanyika katika uwanja uliopo jijini Paris jana Jumatano. Washiriki walijumuisha waigizaji, wanazuoni na wanamuziki.

Mshindi wa tuzo ya Nobel kipengele cha fasihi, Annie Ernaux alisema katika ujumbe wa video, “kuna nyakati katika historia ya taifa ambapo wananchi wake wanafanya uamuzi ambao ni mgumu kuubadili,” akiongeza kuwa “Ni Jumapili ijayo.”

Muungano wa mrengo wa kushoto wa New Popular Front umekuwa nafasi ya pili kwenye duru ya kwanza, na muungano wa vyama tawala unaoongozwa na Rais Emmanuel Macron ulikuwa wa tatu.

Baadhi ya wagombea wameachia ngazi kabla ya duru ya pili Jumapili ijayo ili kuungana vilivyo dhidi ya chama cha mrengo mkali wa kulia. Lakini baadhi ya wanachama wa muungano wa vyama tawala wana mtazamo hasi juu ya ushirikiano huo.