Maswali na Majibu: Tahadhari za kupanda Mlima Fuji (5)

(5) ‘Kupanda kama risasi’

NHK inajibu maswali kuhusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Mlima Fuji, ambao ni mrefu zaidi nchini Japani unavutia wapandaji wengi wakiwemo raia wa kigeni kila mwaka. Lakini msongamano na tabia za kutojali za wapandaji zinasababisha matatizo mbalimbali, hivyo mamlaka zimeanzisha sheria mpya na hatua zingine. Katika mfululizo huu, tutaangazia suala linalojulikana kama “kupanda kama risasi.”

Miongoni mwa sababu zilizofanya mamlaka kuanzisha taratibu mpya ni ongezeko la idadi ya wapandaji wasiokuwa na tabia nzuri. Baadhi yao hujaribu kufanya kile kinachoitwa “kupanda kama risasi,” upandaji wa mlima nyakati za usiku bila kupumzika, ambao unadhaniwa kuwa ni hatari.

Wapandaji wa usiku huelekea kileleni ili kutazama jua likichomoza mlimani, bila kulala katika vibanda vya mlimani. Lakini baadhi yao huwa hawana uzoefu mkubwa wa kupanda, wala vifaa vya kutosha. Huwa wanapata ugonjwa wa mwinuko na ugonjwa wa kushuka kwa halijoto ya mwili. Watu wengi waliokolewa kwa kuwa na dalili kama hizo msimu uliopita wa upandaji. Baadhi yao walilala katika mahema waliyoweka pembeni ya njia ya kupandia, kitu ambacho kimekatazwa, na kufunga njia kwa kupiga kambi hapo. Mwongoza watalii katika eneo hilo anasema wapandaji wa usiku kama risasi ni pamoja na watalii wengi wa kigeni.

Kufuatia hali hiyo, mamlaka zimeamua kufunga geti la kuingilia kwa Njia ya Yoshida mkoani Yamanashi kuanzia saa 10 jioni hadi saa 9 usiku siku inayofuata. Kwa wageni ambao wanapanda mlima kutokea upande wa mkoa wa Shizuoka, maafisa watawauliza wapandaji ambao wanaanza kupanda baada ya saa 10 jioni iwapo wameweka nafasi za vibanda vya mlimani, na kutoa wito kwa wale wasioweka nafasi kujizuia kupanda mlima.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Julai 3, 2024.