Japani yafichua visa vingine vitatu vya unyanyasaji wa kingono vinavyohusisha wanajeshi wa Marekani

Msemaji wa ngazi ya juu wa serikali ya Japani amefichua visa vingine vitatu vya madai ya unyanyasaji wa kingono vinavyohusisha wanajeshi wa Marekani.

Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri Hayashi Yoshimasa alizungumza na wanahabari jana Jumatano baada ya visa viwili vya madai ya unyanyasaji wa kingono katika Mkoa wa Okinawa kufichuliwa.

Wiki iliyopita, ilifichuliwa kuwa mwanajeshi wa Jeshi la Anga la Marekani alifunguliwa mashtaka mwezi Machi kwa madai ya kumteka nyara na kumdhalilisha kingono msichana mwenye umri mdogo mwezi Desemba mwaka jana, na kwamba mwanajeshi wa Jeshi la Majini wa Marekani alifunguliwa mashtaka mwezi uliopita kwa madai ya kujaribu kumnyanyasa mwanamke kingono na kumjeruhi.

Sio tu kwamba matukio haya hayakuwekwa wazi kwa jamii hadi hivi majuzi lakini pia serikali ilishindwa kuwaarifu maafisa wa mkoa kuhusu matukio hayo.

Hayashi alisema kuwa katika mojawapo ya visa vitatu vilivyofichuliwa hivi karibuni, mwanajeshi wa Marekani anashukiwa kufanya mapenzi bila idhini.

Alisema matukio mawili kati ya hayo yanayodaiwa yalitokea mwaka jana Februari na Agosti na lingine linadaiwa kutokea Januari. Alisema hakuna mshukiwa hata mmoja aliyefunguliwa mashtaka.

Hayashi alielezea uhalifu wa ngono unaohusisha wanajeshi wa Marekani kuwa wa kusikitisha sana. Alisema unaleta wasiwasi mkubwa kwa wakazi wa eneo hilo.

Alisema serikali itaendelea kuiomba Marekani kuchukua hatua madhubuti ili kuzuia matukio kama hayo.