Japani yatoa noti mpya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20

Japani leo Jumatano imetoa noti mpya kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20.

Hafla ilifanyika leo Jumatano asubuhi katika makao makuu ya Benki Kuu ya Japani, BOJ katika eneo la Nihonbashi jijini Tokyo.

Gavana wa BOJ Ueda Kazuo alisema kwamba benki hiyo inapanga kuingiza katika mzunguko noti mpya zenye thamani ya yeni trilioni 1.6 ama takribani dola bilioni 9.9 leo Jumatano.

Alisema kwamba wakati miamala isiyotumia fedha taslimu ikizidi kuenea zaidi, anaamini kwamba fedha taslimu itaendelea kuwa na mchango mkubwa kwa kuwa ni njia ya uhakika ya malipo ambayo inaweza kutumika na yeyote, popote na muda wowote.

Chini ya ubunifu mpya wa hivi karibuni, noti hizo zimejumuisha teknolojia mpya ya hologramu ili kuzifanya ziwe ngumu zaidi kughushi. Ofisi ya Taifa ya Kupiga Chapa ilisema hii ni mara ya kwanza teknolojia hiyo imetumika katika noti duniani kote.

Noti hizo pia zina ubunifu kwa watu wote, huku kiasi cha fedha kikionekana kwa ufasaha zaidi katika tarakimu kuliko katika herufi za kanji ili kuzifanya ziwe rahisi kutumika kwa raia wa kigeni.