Maandamano dhidi ya serikali nchini Kenya yasababisha vifo vya watu 39

Makumi ya watu wamefariki nchini Kenya katika maandamano yanayoendelea ambayo yalichochewa mwezi uliopita kutokana na pendekezo la nyongeza ya kodi.

Kikundi cha kutetea haki za binadamu nchini Kenya kinasema kuwa watu 39 walifariki na 361 walijeruhiwa kuanzia Juni 18 hadi Julai 1.

Maandamano yamekuwa yakienea kote nchini Kenya tangu katikati ya mwezi Juni. Mnamo Juni 25, baadhi ya waandamanaji walifanya vurugu na kuvamia eneo la bunge, na kusababisha vikosi vya usalama kufyatua risasi za moto.

Rais wa Kenya William Ruto baadaye alitangaza kuondoa nyongeza ya kodi. Lakini maandamano yanayomtaka ajiuzulu yanaendelea kote nchini humo.

Jana Jumanne, mapigano yalizuka katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi. Polisi wa kutuliza ghasia walirusha mabomu ya machozi na kukabiliana na waandamanaji waliokuwa wakiwarushia mawe.

Kenya ndio kitovu cha uchumi cha Afrika Mashariki. Kampuni nyingi za Kijapani zinafanya shughuli zao nchini humo.

Lakini uchumi wa taifa hilo uliathiriwa zaidi na sababu mbalimbali zikiwemo janga la virusi vya korona na ukame mkali. Serikali ilikuwa inajaribu kurejesha uchumi thabiti kwa kuongeza kodi kwa kiasi kikubwa.

Manung’uniko dhidi ya sera za kiuchumi za serikali bado yapo kwa kiasi kikubwa, hasa miongoni mwa vijana wanaohangaika na kupanda kwa gharama za chakula, mafuta na gharama nyingine za maisha.