Marekani kutangaza mpango wa usaidizi wa usalama wa dola bilioni 2.3 kwa Ukraine

Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin amebainisha kuwa Marekani itatangaza hivi karibuni kwamba itatuma zaidi ya dola bilioni 2.3 nchini Ukraine kama msaada wa kiusalama.

Austin alibainisha mpango huo kabla ya mkutano na Waziri wa Ulinzi wa Ukraine Rustem Umerov. Mkutano huo ulifanyika Wizara ya Ulinzi ya Marekani jana Jumanne.

Austin alisema Marekani "itaendelea kutoa msaada wa uwezo muhimu ambao Ukraine inahitaji ili kukabiliana na uchokozi wa Urusi kwa sasa na kuzuia uchokozi wa Urusi hapo baadaye."

Ubainishaji huo wa Austin unakuja kabla ya mkutano wa viongozi wa NATO huko Washington wiki ijayo. Viongozi watakaohudhuria mkutano huo wanatarajiwa kujadili uungaji mkono kwa Ukraine.

Umerov alielezea shukrani zake kwa msaada huo uliopangwa. Pia alisema kwamba anatazamia kujadili jinsi Ukraine inavyoweza kuwa mwanachama wa NATO katika siku zijazo.