Boti ya uvuvi ya Taiwan yashikiliwa na kikosi cha ulinzi wa pwani cha China

Kikosi cha Ulinzi wa Pwani cha China kimeishikilia boti ya uvuvi ya Taiwan karibu na pwani ya kusini mwa China. Mamlaka za usafiri baharini za Taiwan zinaitaka China kuwaachilia mara moja wafanyakazi hao.

Maafisa wa Kikosi cha Ulinzi wa Pwani cha Taiwan walisema boti hiyo ilisimamishwa kwa ukaguzi wa baharini na meli mbili za serikali ya China kwenye eneo la bahari karibu na Jimbo la Fujian jana Jumanne usiku.

Taiwan ilituma meli mbili za doria kuiokoa boti hiyo, lakini zilizuiwa na idadi kubwa ya meli za Kikosi cha Ulinzi wa Pwani cha China. Boti hiyo ya uvuvi ilipelekwa kwenye bandari ya Fujian.

Maafisa wa Taiwan walisema boti hiyo ilikaguliwa karibu na Visiwa vya Kinmen, ambavyo vipo chini ya udhibiti wa Taiwan.

Inasemekana kuwa boti hiyo ya uvuvi ilikuwa na wafanyakazi sita, wakiwemo wafanyakazi wahamiaji, na ilikuwa ikivua ngisi. Lakini kwa sasa, mamlaka za serikali ya China zimesitisha uvuvi wa ngisi.

Kikosi cha Ulinzi wa Pwani cha Taiwan kinatoa wito kwa China kujiepusha kudhoofisha uhusiano wa pande hizo mbili kupitia hila za kisiasa.