Meya wa Okinawa atafuta mawasiliano mazuri ya kesi zinazowahusu wanajeshi wa Marekani

Meya wa kijiji cha Yomitan mkoani Okinawa Ishimine Denjitsu ametoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Nje kuanzisha tena mfumo wa kushirikishana taarifa kwa haraka kuhusu matukio yanayowahusisha wanajeshi wa Marekani katika mkoa huo uliopo kusini magharibi mwa Japani.

Ishimine alitembelea ofisi ya Wizara ya Mambo ya Nje mkoani Okinawa leo Jumanne. Kambi za jeshi la Marekani zipo kijijini Yomitan.

Wiki iliyopita ilibainishwa kuwa mwanajeshi mmoja wa Kikosi cha Anga cha Marekani mkoani Okinawa alishtakiwa mwezi Machi kwa tuhuma za kumteka na kumnyanyasa kingono msichana mwenye umri mdogo mwezi Desemba mwaka jana.

Pia imebainika kwamba mwanajeshi wa jeshi la majini la Marekani mkoani humo alishtakiwa mwezi Juni kwa kujaribu kumnyanyasa kingono mwanamke mmoja na kumuumiza.

Serikali ya mkoa wa Okinawa haikufahamishwa kuhusu kesi zote mbili.

Tuhuma za uhalifu huo pia zimeibua hasira kwa wenyeji huku mabaraza kadhaa ya manispaa yakiidhinisha maazimio ya malalamishi.

Ishimine amesema mamlaka za eneo hilo hazikutaarifiwa kuhusu kesi ya mwezi Desemba kwa kipindi cha nusu mwaka. Amesema ikiwa taarifa zingeshirikishwa vya kutosha, ingesaidia kuzuia matukio kama hayo kutokea tena.

Balozi wa Wizara ya Mambo ya Nje anayehusika na Masuala ya Okinawa Miyagawa Manabu amesema wizara hiyo inashauriana na ofisi zingine za serikali, ikiwemo mamlaka za uchunguzi kuhusiana na namna ya kupitia upya mfumo wa ushirikishanaji taarifa. Amesema anatumai matokeo yanaweza kuripotiwa haraka iwezekanavyo.