Afisa wa UN aahidi kuendelea kushirikiana na Afghanistan

Afisa mwandamizi wa Umoja wa Mataifa, UN anasema umoja huo umedhamiria kuendelea kushirikiana na Afghanistan inayodhibitiwa na Taliban ili kuangazia vikwazo dhidi ya wanawake na wasichana na masuala mengine yanayoibua mashaka duniani.

Naibu Katibu Mkuu wa UN Rosemary DiCarlo alizungumza na wanahabari jana Jumatatu kufuatia mkutano wa siku mbili kuhusu Afghanistan uliofanyika jijini Doha nchini Qatar.

Taliban ilituma wajumbe kwa mara ya kwanza kwenye mkutano huo wa Doha ambao ni wa tatu wa aina yake. Wajumbe kutoka Marekani, Ulaya, China na Japani pia walishiriki.

DiCarlo alipongeza kuanza kwa mazungumzo ya kina kati ya Taliban na jumuiya ya kimataifa, akiyataja mazungumzo hayo kuwa ya wazi na muhimu.

Taliban imeminya kabisa haki za wanawake tangu iliporejea madarakani mwaka 2021. Wasichana nchini Afghanistan hawaruhusiwi kuendelea na masomo ya sekondari.

Nadhari ni ikiwa Taliban itaendelea kushiriki mazungumzo ya kimataifa.

Msemaji wa Taliban Zabihullah Mujahid, aliyehudhuria mkutano huo, ameelezea msimamo chanya juu ya kujiunga na awamu ijayo ya mazungumzo. Lakini ameongeza kwamba Taliban itakuwa na mtazamo tofauti juu ya kila mkutano, kulingana na ajenda na malengo yake.