Maswali na Majibu: Tahadhari za kupanda Mlima Fuji (4)

(4) Hatua mpya za safari za kupanda mlima katika njia za upande wa Shizuoka

NHK inajibu maswali kuhusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Mlima Fuji, ambao ni mrefu zaidi nchini Japani unavutia wapandaji wengi wakiwemo raia wa kigeni kila mwaka. Lakini msongamano na tabia za kutojali za wapandaji zinasababisha matatizo mbalimbali, hivyo mamlaka zimeanzisha sheria mpya na hatua zingine. Katika mfululizo huu, tunaangazia hatua mpya zinazotekelezwa katika njia za upande wa mkoa wa Shizuoka.

Njia tatu katika upande wa Shizuoka ni Subashiri, Gotemba na Fujinomiya.

Kuanzia msimu huu wa upandaji, mkoa wa Shizuoka umeanzisha mfumo wa majaribio ambao unawaomba wapandaji kusajili kabla taarifa za kibinafsi kwenye tovuti yake ya manispaa. Wapandaji lazima wasajili taarifa ikiwa ni pamoja na ratiba yao ya upandaji, vibanda vya kulala milimani pamoja na kutazama video kuhusu tabia nzuri za upandaji.

Punde ukimaliza kujisajili, unapewa msimbo wa QR ambao unatumiwa katika utepe wa mkononi unaosambazwa mwanzoni mwa safari. Mkoa huo pia unawaomba wapandaji ambao hawajashika nafasi ya vibanda vya kulala mlimani kujizuia kuingia kwenye mlima huo baada ya saa kumi jioni.

Unahitaji kujisajili kupitia tovuti ya manispaa ya Shizuoka. Watumiaji sasa wanaweza wakasajili taarifa zao katika lugha za Kiingereza, Kichina na Kithailand. Mkoa huo unapanga kupanua zaidi usajili hadi lugha zingine ikiwa ni pamoja na Kikorea na Kivietnam.

Kwa wale ambao hawajatangulia kujisajili kabla ya kupanda, unaweza ukaingia kwenye mlima huo kwa kuzingatia taratibu zinazohitajika mwanzoni mwa safari.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Julai 2, 2024.