Mkurugenzi wa hospitali ya Gaza aachiliwa huru na Israel

Israel jana Jumatatu iliwaachilia huru wafungwa wa Kipalestina zaidi ya 50 kutoka kizuizini. Wanajumuisha mkurugenzi wa hospitali ambayo mamlaka zimesema ilitumika kama kituo cha kamandi ya Hamas.

Mamlaka zimesema zimechukua hatua ya kuwaachilia huru ili kupunguza msongamano vizuizini. Mmoja wa waliokuwa kizuizini ni Muhammad Abu Salmiya ambaye ni mkurugenzi wa hospitali ya Al-Shifa. Alikamatwa mwezi Novemba mwaka jana baada ya vikosi vya Israel kuvamia hospitali hiyo.

Baada ya kuachiliwa kwake, Abu Salmiya alisema kulikuwa na mateso karibu kila siku. Alisema vyumba walimokaa vilivamiwa kila siku na wafungwa walipigwa mno. Aliongeza kuwa, “Tunasema haya kwa uhakika kabisa. Tumepitia hayo kwa uchungu mwingi.”

Abu Salmiya alishikiliwa bila kushtakiwa wala kupelekwa mahakamani. Alikana tuhuma kuwa hospitali hiyo ilitumika kwa shughuli za kijeshi.

Wakati huo huo, viongozi wa Israel wamesema vikosi vyao katika eneo la Gaza vimewaua wapiganaji wapatao 20 wakati wa uvamizi kwenye maeneo yanayotumika kutengeneza na kuhifadhi silaha.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu jana Jumatatu alisema jeshi lake lilikuwa linasonga mbele kuelekea hatua ya kutokomeza “jeshi la kigaidi la Hamas.” Ameongeza kuwa vikosi hivyo vitaendelea kushambulia wapiganaji waliosalia.