Mahakama ya Juu ya Marekani yaamua kuhusu kinga ya Trump

Mahakama ya Juu ya Marekani ilitoa hukumu jana Jumatatu kuwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump hawezi kufunguliwa mashtaka kwa “vitendo rasmi” vyoyote alivyofanya kipindi alipokuwa madarakani.

Trump alidai kinga kamili kufuatia vitendo alivyofanya wakati alipokuwa Ikulu na amekuwa akikabiliana na mashtaka katika mahakama ya shirikisho katika juhudi zake za kubadili matokeo ya uchaguzi alioshindwa mwaka 2020, ikiwemo vurugu katika jengo la Bunge.

Mahakama ya juu imeamua kwamba marais wa zamani wana haki ya kupata “kinga kamili” kwa hatua walizochukua wakiwa katika “mamlaka ya kikatiba.” Hata hivyo, imeongeza kwamba katiba haitoi kinga ya kushtakiwa kutokana na vitendo vilivyofanywa “nje ya majukumu ya kikatiba.” Imerudisha kesi hiyo kwenye mahakama ya chini.

Trump amesifia uamuzi huo wa mahakama kwenye mtandao wa kijamii, akielezea kuwa ni “ushindi mkubwa” kwa katiba na demokrasia.

Viongozi wa chama cha Democrat wameita “siku ya huzuni kwa Marekani,” wakisema uamuzi huo ni “fedheha” lakini “haubadilishi ukweli.”

Hata hivyo, uamuzi huo umeondoa matarajio yote ya Trump kushtakiwa kabla ya uchaguzi wa urais mwezi Novemba.