Hungary inayounga mkono Urusi yachukua urais wa zamu wa EU

Hungary, ambayo kwa kiasi kikubwa inachukua msimamo wa kuiunga mkono Urusi, jana Jumatatu ilichukua urais wa zamu wa Baraza la Umoja wa Ulaya, EU. Baadhi ya nchi wanachama zina hisia inayoongezeka ya wasiwasi na mkanganyiko kuhusiana na usimamizi wa sera, kwani Waziri Mkuu wa Hungary Viktor Orban amekuwa akitoa matamshi ya wazi ya kutoiunga mkono Ukraine.

Orban amekuwa akichukua msimamo wa kuipinga EU, na kuegemea mrengo wa kulia na vyama vya kisiasa vya mrengo mkali wa kulia barani Ulaya.

Kauli mbiu yake ya urais huo ni, “Ifanye Ulaya kuwa Kuu Tena,” inayoigiza kauli mbiu inayotumiwa na Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump.

Orban aliandika katika mitandao ya kijamii jana Jumatatu kuwa, “Kila mtu ana furaha kwamba ni zamu yetu ya kuifanya Ulaya kuwa kuu tena!”

Orban alirejelea sera za mabadiliko ya tabia nchi za EU katika makala ya jarida la Financial Times. Alinukuliwa akisema kuwa “EU imekuwa ikiweka malengo yake yenyewe yaliyochochewa kiitikadi bila kutafuta ushauri wa kutosha wa sekta,” na kwamba “kampuni za Ulaya zinapoteza ushindani wake.”

Vyombo vya habari vya Ujerumani vilielezea mashaka juu ya Orban vikiripoti kuwa “Mkosoaji huyo wa EU huenda akapiga breki, hasa inapokuja kwa uungaji mkono wa Ukraine na utawala wa sheria.”

Urais huo huchukuliwa kwa zamu miongoni mwa nchi wanachama wa EU kila baada ya miezi sita, ikimaanisha Hungary itashikilia wadhifa huo hadi mwezi Desemba mwaka huu.