Naibu Waziri Mkuu wa China atumai kuwepo kwa uhusiano mzuri kati ya nchi hiyo na Japani licha ya tukio la kisu

Naibu Waziri Mkuu wa China He Lifeng, katika mkutano na spika wa zamani wa Baraza la Chini la Bunge la Japani Kono Yohei, amesisitiza kuwa uhusiano wa kibiashara wa pande mbili haupaswi kuathiriwa na shambulizi la hivi karibuni lililofanywa na mtu mmoja Mchina dhidi ya raia wa Japani. Ametoa wito kwa kampuni za Japani kufanya uwekezaji zaidi.

He alikaribisha ujumbe wa wanachama 87 kutoka Japani ukiongozwa na Kono mjini Beijing nchini China jana Jumatatu. Wajumbe hao walitoka kwenye Chama cha Uhamasishaji wa Biashara ya Kimataifa cha Japani.

Kulingana na maafisa wa chama hicho, Kono alitoa rambirambi zake kufuatia kifo cha mwanamke mmoja Mchina aliyefariki baada ya kujaribu kumkinga mwanamke Mjapani na mwanawe dhidi ya mshambuliaji huyo aliyekuwa na kisu mjini Suzhou katika jimbo la Jiangsu Juni 24 mwaka huu. Mwanamke huyo Mchina alikuwa mhudumu kwenye basi linalotumiwa na shule moja ya Kijapani.

Kono alitoa wito kwa upande wa China kubaini ikiwa raia wa Japani ndio waliolengwa katika shambulizi hilo.

He alisema aliambiwa na maafisa wa China kuwa shambulizi hilo lilikuwa “tukio la ajali.” Alisisitiza haja ya kuzuia uhusiano wa kibiashara wa pande mbili kuathiriwa na shambulizi hilo.