Urusi yaongeza mashambulizi mashariki mwa Ukraine, vifo vya watoto vyaongezeka

Wizara ya Ulinzi ya Urusi inasema vikosi vya nchi hiyo vimedhibiti vijiji viwili katika eneo la Donetsk mashariki mwa Ukraine.

Jana Jumapili, wizara hiyo ilitangaza kwamba vijiji hivyo ni Spirne na Novooleksandrivka.

Gavana wa Donetsk anasema shambulio la Urusi juzi Jumamosi limeua watu tisa na kujeruhi wengine 16 kwenye eneo hilo.

Urusi inasemekana inajaribu kudhibiti kikamilifu Donetsk. Vikosi vyake vinatarajiwa kusonga zaidi.

Wakati Urusi ikiongeza mashambulizi yake, idadi ya watoto waliouawa na kujeruhiwa Ukraine inaongezeka.

Jana Jumapili, waendesha mashtaka wa Ukraine wamesema watoto 554 wamefariki na wengine zaidi ya 1,419 wamejeruhiwa tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake nchini Ukraine. 550 kati ya waliojeruhiwa ni kutoka Donetsk, na 399 kutoka eneo la Kharkiv, ambako pia ni mashariki mwa Ukraine.