Korea Kusini: Korea Kaskazini yarusha makombora 2 ya balistiki kuelekea kaskazini mashariki

Jeshi la Korea Kusini linasema Korea Kaskazini imerusha makombora mawili ya balistiki kuelekea kaskazini mashariki mapema leo Jumatatu asubuhi.

Wakuu wa Majeshi ya Korea Kusini wamesema makombora hayo yalirushwa kutokea eneo la Jangyon jimbo la Hwanghae Kusini upande wa kusini magharibi mwa Korea Kaskazini, majira ya saa 11:05 alfajiri na saa 11:15 alfajiri.

Wamesema la kwanza lilikuwa ni kombora la balistiki la masafa mafupi lililosafiri umbali wa takribani kilomita 600. La pili lilisafiri umbali wa karibu kilomita 120. Aina ya kombora la pili bado inatathminiwa.

Majeshi ya Korea Kusini na Marekani yanafanya kazi pamoja kutathmini urushaji huo.

Kadhalika Korea Kaskazini ilirusha kombora la balistiki kuelekea Bahari ya Japani Jumatano iliyopita. Ilisema imefanikiwa kufanya jaribio la kutenganisha na kudhibiti mwongozo wa vichwa kadhaa vya makombora. Jeshi la Korea Kusini limekuwa katika tahadhari, likishuku Korea Kaskazini inaweza kurusha kombora lingine la balistiki.