Miezi 6 baada ya tetemeko la Noto: Watu zaidi wanahofiwa kufariki kutokana na msongo wa mawazo na uchovu baada ya janga

Leo Jumatatu inatimia miezi sita tangu tetemeko kubwa la ardhi lilipoikumba Rasi ya Noto mkaoni Ishikawa na maeneo ya karibu katikati mwa Japani. Idadi ya vifo kutokana na sababu za baada ya janga inaweza kuongezeka zaidi.

Maafisa wamethibitisha kuwa tetemeko hilo la ukubwa wa 7.6 katika kipimo cha Richter limesababisha vifo vya watu 281 na wengine watatu hawajulikani waliko katika mkoa huo.

Idadi hiyo ya vifo inajumuisha watu 52 waliofariki baada ya kuugua kutokana na sababu za baada ya janga, ikiwa ni pamoja na uchovu na msongo wa mawazo.

Watu wengi zaidi wanahofiwa kufariki kutokana na sababu hizo kwa kuwa wakazi wengi waliopoteza makazi yao katika tetemeko hilo hawana namna ila kuishi katika nyumba za muda au makazi mengine ya muda.

Wataalam wanatoa wito kwa serikali za mitaa na makundi ya sekta binafsi kufanya kazi pamoja ili kuwapa waliohamishwa msaada wa kina, kama vile ufuatiliaji wa mtindo wa maisha na huduma za uuguzi.

Maafisa wanakadiria kuwa majengo 22,000 katika maeneo yaliyokumbwa na tetemeko hilo yanahitaji kubomolewa na vifusi kuondolewa na manispaa za maeneo hayo kwa niaba ya wamiliki. Lakini utaratibu huo umekamilika kwa takriban asilimia 4 tu, au takriban majengo 900 kati ya hayo.