Zelenskyy ataja ‘mpango wa kina’ kufikia mwishoni mwa mwaka kumaliza mgogoro

Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine ameashiria kwamba mpango wa kumaliza mgogoro na Urusi utaandaliwa kufikiwa mwishoni mwa mwaka huu.

Alisema juzi Ijumaa jijini Kyiv kwamba “ni muhimu kwa sisi kuonesha mpango wa kumaliza vita utakaoungwa mkono na sehemu kubwa ya dunia.”

Zelenskyy alisisitiza umuhimu wa kuzuia uchokozi wa Urusi kwa nguvu, huku maandalizi yakifanyika kwa mpango wa amani.

Alisema kwamba “kuwa imara kwenye uwanja wa vita na kuendeleza mpango wa wazi na wa kina” vitapaswa kufanywa sambamba.

Hakuzungumzia juu ya taarifa za kina. Kuna fununu kuwa mpango huo utachochea majadiliano kwenye mikutano ijayo ya viongozi wa kimataifa juu ya kurejesha amani kwa Ukraine.

Urusi kwa upande mwingine, inadai kwamba Ukraine iondoe vikosi vyake kutoka maeneo manne ambayo iliyatwaa kwa upande mmoja kama sharti la kuanza kwa majadiliano ya amani.