Ukandamizaji uhuru wa kuzungumza waongezeka katika eneo la Hong Kong chini ya sheria za usalama wa taifa

Leo Jumapili inaadhimishwa miaka minne tangu sheria ya usalama wa taifa ya China kwa eneo la Hong Kong kuanza kufanya kazi. Sheria hiyo imetungwa ili kuwasaka wanaopinga shughuli za serikali.

Ukandamizaji wa uhuru wa kuzungumza umeongezeka mwaka huu baada ya mamlaka za eneo hilo kuanza kuitekeleza sheria hiyo kuanzia mwezi Machi.

Sheria hiyo ya usalama ilianza kufanya kazi mwezi Juni 30, 2020, takribani mwaka mmoja baada ya maandamano makubwa ya kuipinga kuzuka Hong Kong.

Chini ya sheria hiyo, wanasiasa na wanaharakati wanaopendelea demokrasia wamekuwa wakikamatwa, na maandamano ya kuipinga serikali yamekuwa yakizuiliwa.

Mwezi uliopita, wanaharakati 14 wanaopendelea demokrasia walihukumiwa kwa tuhuma za kukiuka sheria hiyo. Walikuwa ni miongoni mwa wanaharakati 47, ikiwa ni pamoja na wabunge wa zamani wanaopendelea demokrasia ambao walishitakiwa kwa kudhoofisha mamlaka miaka mitatu iliyopita.

Kesi mahakamani inaendelea kwa washitakiwa wengine, na kuongeza kushikiliwa kwao.

Sheria ya eneo hilo ambayo ilianza kufanya kazi mwezi Machi inawatia hatiani watu wenye makosa ya uhaini na uingiliwaji wa taasisi za kigeni. Pia inaelezea adhabu kali kwa vitendo ambavyo vinachochea chuki dhidi ya serikali ya China.

Mapema mwezi huu, mwanaume mmoja alishitakiwa kwa kukiuka sheria hiyo akituhumiwa kuvaa fulana yenye ujumbe uliotumika katika maandamano ya mwaka 2019.

Mamlaka za usalama katika eneo la Hong Kong ziliiambia NHK kuwa katika kipindi cha miaka minne watu 299 wamekamatwa kwa tuhuma za kuhatarisha usalama wa taifa.