Putin aashiria kurejesha utengenezaji wa makombora ya masafa mafupi na ya kati

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema nchi yake inahitaji kurejesha utengenezaji wa makombora ya masafa mafupi na ya kati yenye uwezo wa kubeba silaha za nyuklia, na kisha kufikiria mahali pa kuyapeleka.

Akizungumza kwenye mkutano wa mtandaoni wa Baraza la Usalama la Urusi juzi Ijumaa, Putin alisema nchi hiyo inahitaji kuanza kutengeneza makombora na kuamua mahali pa kuyaweka ili kuhakikisha usalama wa nchi hiyo.

Alielezea kuwa pendekezo hilo lilikuwa ni hatua za kukabiliana na Marekani, ambayo imepeleka makombora hayo katika mataifa ikiwa ni pamoja na Denmark kwa ajili ya mazoezi ya kijeshi.

Taasisi ya Masomo ya Vita imesema, “Putin huenda akawa anatumia mazoezi haya kama njia ya kukwepa lawama kwenye kampeni yake kubwa ya udhibiti iliyolenga kuvunja moyo msaada wa kijeshi wa nchi za Magharibi kwa Ukraine.

Jopo la ushauri la kitaalam la Marekani pia limesema, “Ikulu ya Urusi imeweka hofu ya mzozo wa silaha za nyuklia kati ya Urusi na nchi za Magharibi katika uvamizi wake wote ili kuzifanya nchi za Magharibi kuogopa kuipatia Ukraine silaha inazohitaji kuhimili ulinzi wake dhidi ya vikosi vya Urusi.”

Chini ya Mkataba wa Makombora ya Nyuklia ya Masafa ya Kati, Marekani na Urusi zilikubaliana kutomiliki, kutotengeneza ama kujaribu makombora ya ardhini ama angani yenye umbali wa kilomita 500 hadi 5,500.

Mkataba huo ulimaliza muda wake mwaka 2019. Urusi imesema haitotengeneza ama kupeleka makombora hadi pale Marekani itakapofanya hivyo.