Mfalme na Mkewe wahitimisha ziara yao nchini Uingereza kwa kuzuru Chuo Kikuu cha Oxford

Mfalme wa Japani Naruhito na Mkewe Masako wamehitimisha ziara yao nchini Uingereza kwa kuzuru Chuo Kikuu cha Oxford, ambapo wote wawili walisoma wakiwa vijana.

Wawili hao walizuru viwanja vya Balliol College jana Ijumaa. Mke wa Mfalme alisoma hapo kwa miaka miwili wakati huo akifanya kazi katika Wizara ya Mambo ya Nje.

Wanandoa hao wa Kifalme baadaye walihudhuria chakula cha mchana kilichoandaliwa na kansela wa chuo hicho, na hafla ambapo shahada ya heshima ilitolewa kwa Mke wa Mfalme.

Mfalme pia alisoma Oxford kwa miaka miwili, katika Merton College. Tajiriba ya kuishi na wanafunzi wengine 150 kwenye mabweni inaonekana ilikuwa na matokeo makubwa kwenye maisha yake. Kwenye kumbukumbu yake, aliandika kwamba alifurahia uhuru wa kiwango cha juu ambao asingeupata nchini Japani, kwenda kwenye mabaa na disko pamoja na marafiki.

Mfalme aliwashukuru watu wa Uingereza kwa maneno yao mazuri na ukarimu.

Alisema: “Ninahisi kama nimerejea kwenye sehemu iliyodumu kwenye fikra zangu. Nilifurahia kusikia watu wengi sana wakisema, ’Karibu tena!’ Uingereza pia ni sehemu ya kumbukumbu kwa Masako, hivyo tumefurahi sana kuwa hapa pamoja.”

Mfalme pia alisema anatumai ziara yao itaimarisha urafiki kati ya Japani na Uingereza.