Wanachama wa Baraza la Usalama la UN waelezea wasiwasi wao juu ya mkataba mpya wa Urusi na Korea Kaskazini

Wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC wameelezea wasiwasi wao juu ya mkataba mpya uliosainiwa kati ya Urusi na Korea Kaskazini kwamba utaimarisha ushirikiano wa kijeshi wa pande mbili.

UNSC iliitisha mkutano wa dharura jana Ijumaa kwa maombi ya Japani, Marekani na nchi zingine.

Mkataba huo mpya kati ya Urusi na Korea Kaskazini unabainisha kwamba iwapo nchi mojawapo itakuwa katika hali ya vita, nchi nyingine itatoa msaada wa kijeshi na mingineyo.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa UN na Mwakilishi Mkuu wa Masuala ya Kuondokana na Silaha Nakamitsu Izumi alibainisha kuwa usafirishaji silaha kutoka Korea Kaskazini unakiuka maazimio ya UNSC.

Alisema nchi zote, ikiwemo Urusi, “zinapaswa kutekeleza ipasavyo vikwazo vya UNSC” kwa Korea Kaskazini.

Balozi wa Japani UN Yamazaki Kazuyuki alisema Japani “inashutumu kwa maneno makali iwezekanavyo” usafirishaji wa makombora ya balistiki wa Korea Kaskazini kwa Urusi katika kukiuka maazimio ya Baraza la Usalama, pamoja na Urusi kutumia silaha hizo dhidi ya Ukraine. Aliongeza kwamba usafirishaji wa silaha hizo utazidisha mzozo nchini Ukraine.”

Balozi wa Urusi UN, Vassily Nebenzia, aliziita fununu juu ya Urusi kutumia makombora ya Korea Kaskazini kuwa si za kweli.

Balozi wa Korea Kaskazini UN, Kim Song, aliunga mkono maoni hayo. Alisema hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi juu ya mkataba huu iwapo hakuna nia ya kuzivamia Korea Kaskazini na Urusi.