Watu wa Okinawa waandamana juu ya shutuma za visa vya shambulio la kingono vinavyohusisha vikosi vya Marekani

Watu wa Okinawa wamejitokeza kwa nguvu kupinga mfululizo wa visa vya madai ya unyanyasaji wa kingono vinavyohusisha maafisa wa jeshi la Marekani katika mkoa huo uliopo kusini magharibi mwa Japani.

Kundi la takribani watu 100 walikusanyika jana Ijumaa mbele ya Kambi ya Kadena ya Jeshi la Anga la Marekani. Kundi moja la eneo hilo linalofanyia kazi kuondoa unyanyasaji wa kijinsia hapo awali lilitoa wito kwa watu kuandamana.

Visa viwili vinavyohusisha maafisa wa jeshi la Marekani katika mkoa wa Okinawa vilibainika juma hili.

Ilibainika kwamba afisa wa Jeshi la Anga la Marekani alishtakiwa mwezi Machi mwaka huu kwa kushukiwa kumteka na kumshambulia kingono msichana wa umri mdogo mwezi Disemba mwaka jana.

Katika kisa kingine, mwanajeshi wa jeshi la wanamaji alishutumiwa kwa kujaribu kumshambulia kingono mwanamke.

Muandaaji wa maandamano hayo alionekana akiwaambia waandamanaji wengine kwamba hawezi kukaa kimya juu ya matukio hayo.