Maswali na Majibu: Tahadhari za kupanda Mlima Fuji (2)

(2) Kanuni mpya

NHK inajibu maswali yanayohusiana na namna ya kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Mlima Fuji, ambao ni mlima mrefu zaidi nchini Japani, huvutia wapanda mlima wengi kila mwaka wakiwemo raia wa kigeni. Hata hivyo, msongamano wa watu pamoja na tabia za wapanda mlima za kutozingatia kanuni zinasababisha matatizo mbalimbali, kwa hiyo mamlaka zimetambulisha kanuni mpya na hatua zingine. Katika kipengele hiki, tunaangazia kaununi mpya zitakazoanzishwa kwenye Njia ya Yoshida mkoani Yamanashi.

Wakati wa msimu wa kupanda mlima katika majira ya joto mwaka 2023, wapanda mlima takribani 140,000 walipita Njia ya Yoshida, ambayo ni takribani asilimia 60 ya wapanda mlima wote kwenye mlima huo.

Mkoa wa Yamanashi umeanzisha kanuni mpya kwenye Njia ya Yoshida msimu huu kuanzia Julai mosi. Lango limewekwa kwenye kituo cha tano kilichopo kwenye urefu wa mita 2,300 kutoka usawa wa bahari, ili kudhibiti idadi ya wapanda mlima kutozidi 4,000 kwa siku. Lango hilo hufungwa kati ya saa kumi jioni hadi saa tisa usiku.

Wapanda mlima wanaotumia Njia ya Yoshida watatakiwa kulipa ada ya yeni 2,000, au takribani dola 13 kila mtu. Wanaweza wakalipa ada hiyo langoni hapo au kufanya malipo mtandaoni kabla ya kuanza safari ili kusiwe na vikwazo katika safari yao.

Mfumo mpya wa kushika nafasi pia umeanzishwa kwa Njia ya Yoshida. Tutatoa taarifa za kina katika kipengele kijacho.

Taarifa hii ni sahihi hadi kufikia Juni 28, 2024.