Wizara ya viwanda ya Japani kuyataka makampuni ya mitandao ya kijamii kukabiliana na tatizo la matangazo bandia

Wizara ya viwanda ya Japani inapanga kuyataka makampuni makubwa ya TEHAMA kuchukua hatua ili kuzuia matangazo bandia yasirushwe kwenye majukwaa yao.

Hatua hiyo inajiri huku kukiwa na ongezeko la visa vya ulaghai unaofanywa na waigaji wa watu mashuhuri kwenye matangazo ya mitandao ya kijamii wakiomba uwekezaji. Majina na picha za watu mashuhuri hutumiwa katika matangazo kama haya bila idhini yao.

Wizara hiyo imezihoji kampuni za Google, LY Corporation na Meta, wanaoendesha Facebook, kuhusu matangazo bandia kwenye mitandao ya kijamii, na kutoa matokeo ya utafiti huo.

Wizara imegundua kuwa kampuni za TEHAMA zilipokea, katika kipindi cha miezi 3 tangu Machi, makumi ya maelfu ya ripoti kuhusu matangazo bandia na maombi ya kuyafuta.

Wizara ilizihoji kampuni hizo kuhusu mchakato wao wa kukagua ili kuzuia matangazo bandia yasirushwe.

Iligundua kuwa ni kampuni ya Meta iliyothibitisha utambulisho wa mtangazaji ikiwa chapisho la mtu linahusiana na mada fulani, kama vile matatizo ya kijamii na uchaguzi.

Kampuni za Google na LY Corporation zilisema zinachunguza matangazo kwa mjumuisho wa macho na mashine, huku Meta ikijibu kuwa inafanya hivyo hasa kwa mashine.

Wizara inasema ina wasiwasi kwamba kampuni ya Meta hutatua tatizo ikiwa tu litasababisha uharibifu unaoonekana, na kwamba ukaguzi wa utambulisho unaofanywa na Meta unaweza kuwa hautoshi.

Wizara inapanga kuyataka makampuni kujibu malalamiko na maombi ya kufutwa ipasavyo na kuyaonyesha katika uchunguzi wao.