Ndugu wa mateka wa Japani wazungumza kwenye kongamano la Umoja wa Mataifa

Ndugu wa raia wa Japani waliotekwa na Korea Kaskazini walizungumza kwenye kongamano la Umoja wa Mataifa lililofanyika kwa njia ya mtandao. Wametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kufanya kazi pamoja kutatua suala hilo.

Tukio hilo la jana Alhamisi liliandaliwa na Japani, Marekani, Australia, Korea Kusini pamoja na Umoja wa Ulaya. Washiriki walikuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri la Japani Hayashi Yoshimasa, ambaye pia anahudumu kama waziri anayeshughulikia suala la mateka hao.

Yokota Takuya, ambaye ni kiongozi wa kundi la familia za mateka wa Japani, alizungumza kwenye kongamano hilo. Dada yake mkubwa aitwaye Megumi, alitekwa mnamo mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 13.

Yokota alisema kuna ukomo wa muda katika kutatua suala hilo kwa kuwa ni wazazi wawili pekee wa mateka waliosalia ambao bado wapo hai.

Alisema wazazi hao ni mama wa Megumi aitwaye Yokota Sakie mwenye umri wa miaka 88 na Arimoto Akihiro mwenye umri wa miaka 95 ambaye ni baba wa mateka mwingine Arimoto Keiko.

Serikali ya Japani inasema raia wasiopungua 17 walitekwa na mawakala wa Korea Kaskazini miaka ya 1970 na 1980. Watano walirejea nchini Japani baada ya mkutano wa viongozi wakuu wa nchi hizo mnamo mwaka 2002. Lakini mateka wengine 12 bado hawajulikani walipo.