Chama cha Kikomunisti cha China chaamua kuwafukuza mawaziri wawili wa zamani wa ulinzi

Shirika la habari la serikali ya China la Xinhua linasema Chama cha Kikomunisti kimeamua kuwafukuza mawaziri wawili wa zamani wa ulinzi kwa kukiuka mno nidhamu yake na sheria ya nchi hiyo.

Shirika hilo linasema uongozi wa chama hicho ulifanya uamuzi unaowahusu Waziri wa zamani wa Ulinzi Li Shangfu na mtangulizi wake Wei Fenghe jana Alhamisi.

Aidha, linasema kamati ya nidhamu na usimamizi ya Tume Kuu ya Kijeshi ilianzisha uchunguzi dhidi ya Li na Wei mwaka jana.

Shirika la Xinhua linasema uchunguzi ulibaini kuwa wawili hao walitumia nyadhifa zao kuwatafutia wengine mafao na walipokea kiwango kikubwa cha fedha na vitu vya thamani.

Xinhua inaripoti kuwa Ofisi ya Kisiasa ya chama hicho imeamua kuhamisha kesi za jinai zinazoshukiwa hadi kwa taasisi husika katika jeshi kwa ajili ya uchunguzi kufanywa na mashtaka kufunguliwa.

Shirika hilo linasema vitendo vyao vilileta madhara makubwa kwa uendelezaji wa ulinzi wa taifa na vikosi vya jeshi. Lakini hakuna maelezo ya kina yametolewa.

Mwezi Desemba mwaka jana, China iliwaondoa maafisa tisa wa ngazi za juu wa jeshi kutoka kwenye taasisi yake ya juu ya kutunga sheria ambayo ni Bunge la Taifa la Watu. Mwezi huo huo, maafisa watendaji watatu waandamizi wa kampuni zenye uhusiano na jeshi zinazomilikiwa na serikali pia walifukuzwa kutoka taasisi ya juu ya ushauri ambayo ni Kongamano la Ushauri wa Kisiasa la Watu wa China.

Baadhi ya vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na Hong Kong viliripoti wakati huo kuwa kufukuzwa kwao kunaweza kuwa kulitokana na uchunguzi wa ufisadi katika manunuzi yaliyofanywa na Kikosi cha Roketi cha jeshi ambacho kinasimamia silaha za nyuklia na makombora.

Rais wa China Xi Jinping alitumia mkutano wa kijeshi wiki jana kusisitiza dhamira yake ya kuendelea na msako mkubwa dhidi ya ufisadi.