Maswali na Majibu: Tahadhari ya kupanda Mlima Fuji (1)

(1) Msimu wa kupanda mlima na njia

NHK inajibu maswali kuhusiana na kuhakikisha usalama katika maisha ya kila siku. Mlima Fuji, ambao ni mlima mrefu zaidi nchini Japani, unavutia wapandaji wengi kila mwaka, wakiwemo raia wa kigeni. Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, msongamano kwenye njia za kupandia mlima huo na tabia mbaya za baadhi ya wapandaji zimezua wasiwasi. Mamlaka zinachukua hatua kushughulikia matatizo hayo, kama vile kutambulisha miongozo mipya kwa wapandaji. Katika mfululizo huu, tutakuwa tunakujuza kile ulichopaswa kufahamu kabla ya kupanda Mlima Fuji.

Ukiwa na urefu wa mita 3,776, Mlima Fuji ndiyo mlima mrefu zaidi nchini Japani. Umetengwa na UNESCO kama eneo la Urithi wa Kiutamaduni Duniani. Kuna njia nne za kufika kileleni. Kila mwaka, njia ya upande wa Mkoa wa Yamanashi hufunguliwa kwa wapandaji Julai mosi na njia tatu katika upande wa Mkoa wa Shizuoka Julai 10. Njia zote hufungwa Septemba 10.

Wizara ya Mazingira inasema kwamba mlima huo huvutia jumla ya wapandaji 221,000 katika kipindi hicho cha msimu uliopita wa joto, ikirejea karibu kiwango sawa na mwaka 2019, kabla ya janga la korona. Lakini msongamano kwenye njia za kupanda mlima na tabia mbaya za wapandaji zimesababisha mamlaka za maeneo husika kutambulisha sheria mpya. Hizi ni pamoja na mfumo wa kuweka nafasi mtandaoni na kukusanya ada kutoka kwa wapandaji. Katika awamu inayofuata, tutakuwa tunakupatia taarifa muhimu kwa wapandaji, kwa kila njia ya kupandia.

Taarifa hii ni hadi kufikia Juni 27, 2024.