Wapandaji wanne wa Mlima Fuji wafariki kabla ya njia kufunguliwa

Mamlaka nchini Japani zimewaonya watu kutopanda Mlima Fuji kabla ya kuwa salama kufanya hivyo. Zimeshuhudia wapandaji wanne wakipoteza maisha ilihali njia bado zimefungwa kwa wapandaji.

Polisi walipigiwa simu Jumapili asubuhi kutoka kwa mkazi wa Tokyo ambaye hakuweza kuwasiliana na mume wake mwenye umri wa miaka 53 baada ya kwenda kupanda Mlima Fuji.

Polisi walikwenda kumtafuta na kukuta watu watatu wengine wakiwa wamepata ugonjwa wa moyo kusimama karibu na bonde upande wa kusini wa kilele cha mlima huo.

Wapandaji hao walipatikana katika maeneo tofauti. Polisi wanafanya kazi ya kuwatambua na kubaini jinsi walivyofariki.

Njia tatu kutoka Mkoa wa Shizuoka na moja kutoka mkoa wa Yamanashi hazijafunguliwa kwa msimu huu hadi Julai. Lakini hiyo haiwazuii baadhi ya watu kupanda mlima.

Takekawa Shunji, mwongoza watu katika milima ya ndani na nje ya Japani, alielezea changamoto za kupanda Mlima Fuji.

Alisema: “Mlima Fuji wakati wa majira ya baridi kali huorodheshwa kuwa mojawapo ya milima migumu zaidi nchini Japani kupanda. Hali ni mbaya sana kwa watu walio na uzoefu fulani na milima ya kawaida wakati wa msimu wa baridi hawawezi kukabiliana nayo. Bado kuna theluji mwezi Juni, kwa hivyo mpandaji lazima ajue kwamba hali hazitakuwa tofauti na zile za msimu wa baridi.

Maafisa wanasema kwamba kupanda kabla ya msimu wake ni hatari. Wanawasihi watu wasijaribu kufanya hivyo.