Wanajeshi wadhibiti kwa muda uwanja wa katikati mwa La Paz nchini Bolivia

Vikosi vyenye silaha viliudhibiti kwa muda uwanja wa katikati mwa mji wa La Paz nchini Bolivia katika jaribio la hivi karibuni la mapinduzi ya kijeshi jana Jumatano. Baadhi ya wanajeshi walilazimisha kuingia ikulu. Waliripotiwa kuondoka baadaye.

Picha za video zinaoonyesha wanajeshi kadhaa na magari ya kivita yakikusanyika huko Plaza Murillo, ambapo majengo muhimu kama vile ikulu na bunge yapo.

Pia zinaonyesha gari lenye silaha likigonga sehemu ya kuingilia ikulu na wanajeshi wakiingia ndani kwa haraka.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo viliripoti kwamba vikosi hivyo viliondoka baada ya mkuu mpya wa majeshi aliyeteuliwa na Rais Luis Arce kuwataka warejee kwenye vitengo vyao.

Ripoti zinasema mmoja wa makamanda wa jeshi alifutwa kazi juzi Jumanne na kuelezea kutoridhishwa kabisa na utawala wa sasa.

Mamlaka za nchi hiyo zinasema zimemkamata kamanda huyo wa zamani kwa kushukiwa kupanga jaribio la mapinduzi.