Korea Kaskazini inasema ilifanikiwa kufanya jaribio la uwezo wa kombora la vichwa vingi

Korea Kaskazini inasema imefanikiwa kufanyia majaribio uwezo wa kombora lenye vichwa vingi.

Korea Kaskazini imesema leo Alhamisi kwamba Idara yake ya Makombora "kwa mafanikio ilifanya jaribio la kutenganisha na kudhibiti mwongozo wa kila kichwa kinachojongea" jana Jumatano.

Tangazo hilo lilitolewa kupitia gazeti la Chama tawala cha Wafanyakazi nchini humo na vyombo vingine vya habari.

Pia tangazo hilo lilisema jaribio hilo lilifanywa kwa kutumia injini ya hatua ya kwanza ya kombora la balistiki la masafa ya kati linalotumia fueli mango ndani ya umbali wa nusu kipenyo cha kilomita 170 hadi 200.

Tangazo hilo liliongeza kuwa vichwa vya kombora linalojongea vilivyotenganishwa viliongozwa kwa usahihi katika maeneo lengwa matatu yaliyoratibiwa.

Jana Jumatano Jeshi la Korea Kusini lilisema kwamba Korea Kaskazini ilirusha kombora la balistiki kutoka eneo la ndani au karibu na Pyongyang, lakini urushaji huo unaonekana haukufanikiwa.