Erdogan amshutumu Netanyahu kwa kugeuzia macho kwenye vita dhidi ya Hezbollah

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ameshutumu maoni ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yalioashiria kwamba ataongeza mapambano dhidi ya kundi la Waislamu wa Shia la Hezbollah lenye makao yake nchini Lebanon.

Netanyahu alikiambia chombo kimoja cha habari cha nchini Israel Jumapili iliyopita kwamba nchi hiyo inakaribia kumaliza awamu ya mapigano makali dhidi ya Hamas katika Ukanda wa Gaza. Aligusia juu ya kupeleka vikosi zaidi kwa mapigano dhidi ya Hezbollah.

Erdogan alisema jana Jumatano kwamba Israel imeiteketeza Gaza na sasa inaonekana kuelekeza macho yake kwa Lebanon. Pia alisema mpango wa Netanyahu kueneza vita utasababisha janga.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, aliyezuru katika nchi za Israel na Lebanon juma hili, alielezea wasiwasi wake juu ya mapigano ya Israel na Hezbollah kwenye mahojiano na chombo cha habari kimoja cha Ujerumani jana Jumatano.

Alisema kitu cha msingi zaidi ni kutumia njia zote za kidiplomasia, na kwamba Ujerumani inashirikiana na nchi ikiwemo Marekani kupunguza mvutano.

Katika onyo la dhahiri kwa Hezbollah, ofisi ya waziri mkuu wa Israel ilisema jana Jumatano kuwa Netanyahu alikagua mazoezi ya kijeshi yaliyofanyika jirani na mpaka na Lebanon.