Mawaziri wa Ulinzi wa Marekani na Urusi wawasiliana kwa simu

Mawaziri wa Ulinzi wa Marekani na Urusi wamezungumza kwa njia ya simu kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miezi 15.

Serikali za Marekani na Urusi zinasema Waziri wa Ulinzi wa Marekani Lloyd Austin na mwenzake wa Urusi Andrei Belousov, walifanya mkutano kwa njia ya simu jana Jumanne. Simu ilipigwa na Austin.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani inasema Austin "alisisitiza umuhimu wa kudumisha njia za mawasiliano wakati ambapo vita vya Urusi dhidi ya Ukraine vinaendelea."

Wizara ya Ulinzi ya Urusi inasema mawaziri hao walibadilishana mawazo kuhusu hali ya Ukraine.

Inasema pia kwamba Belousov aliangazia hatari ya kuongeza mzozo kwa sababu ya Marekani kuendelea kuvipatia silaha vikosi vya Ukraine.

Mara ya mwisho mawaziri wa ulinzi wa nchi hizo mbili kuzungumza ilikuwa Machi mwaka 2023. Mazungumzo ya simu ya jana Jumanne yalikuwa ya kwanza kati ya Austin na Belousov, ambaye aliteuliwa kuwa waziri wa ulinzi mwezi Mei.