Waandamanaji wanaopinga ongezeko la kodi wavamia bunge la Kenya, vifo vyaripotiwa

Waandamanaji wanaopinga pendekezo la nyongeza ya kodi nchini Kenya wamevamia bunge. Mapambano na polisi yanasemekana kusababisha vifo.

Waandamanaji walivamia katika majengo ya bunge jijini Nairobi jana Jumanne wakati wabunge walipokuwa wakijadili mswada wa nyongeza kubwa ya kodi.

Vyombo vya habari vya nchi hiyo vinaripoti kwamba baada ya mswada huo kupitishwa, waandamanaji walivuka vizuizi vya polisi na kuingia ndani ya jengo la bunge kwa nguvu. Inasemekana moto ulizuka katika sehemu ya jengo hilo.

Kuna ripoti kwamba polisi waliwafyatulia risasi za moto waandamanaji. Shirika la habari la Reuters linasema mwanahabari wake alishuhudia miili isiyopungua mitano karibu na bunge.

Maandamano ya kupinga mswada huo unaoungwa mkono na serikali yamefanyika kote nchini Kenya. Uchumi wa Kenya umeathiriwa na janga la virusi vya korona, kupanda kwa bei za vyakula kulikosababishwa na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na ukame mkali ndani ya nchi.