Mkuu wa jeshi la Israel asema operesheni ya Rafah inakaribia kumalizika

Mnadhimu Mkuu wa jeshi la Israel Luteni Jenerali Herzi Halevi ameashiria kuwa operesheni ya ardhini ya jeshi hilo kusini mwa Gaza inakaribia kumalizika.

Vikosi vya Ulinzi vya Israel juzi Jumatatu vilitoa uchambuzi wa Halevi kuhusu operesheni ya Rafah.

Halevi alisema, “Tuna viwango vya juu sana vya mafanikio kutoka kwenye mapambano ya Rafah.” Aliongeza kuwa, “Tunakaribia kwa hakika wakati ambao tunaweza kusema tumeharibu Brigedi ya Rafah,” akizungumzia vikosi vya Hamas katika mji wa Rafah.

Hamas hata hivyo, jana Jumanne ilisema katika mitandao ya kijamii kuwa ililishambulia jeshi la Israel katika mji wa Rafah. Kundi hilo linasisitiza kuwa Israel inakataa mapendekezo katika majadiliano ya kusitisha mapigano na kuachiwa kwa mateka.