Serikali ya China: Shambulio la kisu kwa basi la shule ya Kijapani lilikuwa ni ‘tukio la kipekee’

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Mao Ning anasema uchunguzi wa awali wa polisi unaashiria kuwa shambulizi la kisu lililotokea juzi Jumatatu katika kituo cha basi la shule ambalo lilijeruhi mwanamke mmoja wa Kijapani na mwanaye lilikuwa ni “tukio la kipekee.”

Akizungumza katika mkutano na wanahabari jana Jumanne, Mao pia alisema tukio hilo ni la kusikitisha.

Alisema serikali itaendelea kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha usalama kwa raia wote wa kigeni.

Tukio hilo lilitokea katika mji wa mashariki wa Suzhou katika jimbo la Jiangsu. Mwanaume mmoja mwenye kisu alishambulia basi la shule ya Kijapani lililokuwa limebeba wanafunzi. Alimjeruhi mwanamke na mwanaye ambao walikuwa katika kituo cha basi.

Mhudumu wa basi raia wa China pia alichomwa kisu. Aliripotiwa kuwa katika hali mbaya.

Polisi katika eneo hilo walifichua tukio hilo jana Jumanne mchana na kusema walimkamata mwanaume mwenye umri wa miaka 52. Walisema hivi karibuni mtuhumiwa huyo alihamia Suzhou kutoka eneo lingine na hana ajira. Lakini polisi hawakutoa taarifa zaidi, ikiwa ni pamoja na sababu za kutokea kwa tukio hilo.