Mitsui yajiunga na mradi wa UAE wa kuzalisha amonia kuanzia mwaka 2027

Mradi katika Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE unaohusisha kampuni ya kibiashara ya Kijapani ya Mitsui & Co. unapanga kuanza kuzalisha amonia kuanzia mwaka 2027.

Amonia inachukuliwa kuwa chanzo cha nishati cha kizazi kijacho kwani haizalishi gesi ya kabonidioksidi inapochomwa.

Mradi huo unaongozwa na kundi la nishati la ADNOC ambalo linamilikiwa na serikali ya UAE.

Vyanzo vya habari vinasema utaanza kuzalisha tani milioni moja za amonia kila mwaka kuanzia mwaka 2027.

Kampuni ya Mitsui inapanga kusafirisha sehemu ya amonia hiyo hadi nchini Japani na nchi zingine za bara Asia. Fueli hiyo itatumiwa katika meli na uzalishaji wa umeme.