Urusi yamuita balozi wa Marekani juu ya shambulizi eneo la Crimea

Wizara ya Mambo ya Nje ya Urusi jana Jumatatu ilimuita balozi wa Marekani nchini humo Lynne Tracy kufuatia shambulizi lililosababisha vifo katika eneo la Crimea lililofanywa na Ukraine. Wizara ya Ulinzi ya Ukraine imesema makombora ya masafa marefu ya ATACMS yaliyowekwa vichwa vya mabomu ya kishada yalitumika.

Mamlaka zilizowekwa na Urusi mjini Sevastopol zilisema shambulizi hilo la juzi Jumapili liliua watu wanne na kujeruhi wengine 153 wakiwemo watoto.

Wizara ya Mambo ya Nje ilimwaambia balozi huyo kuwa Marekani hakika imekuwa sehemu ya mgogoro huo kwa kuipatia Ukraine silaha za kisasa zaidi.

Wizara hiyo pia ilisema Marekani inabeba “jukumu sawa” na Ukraine kufuatia shambulizi hilo. Ilionya kuwa “ni bayana hatua za kulipiza kisasi zitafuata.”

Mshauri wa Rais wa Ukraine Mykhailo Podolyak alitetea shambulizi hilo akisema jana Jumatatu kuwa Crimea bila shaka ni eneo lililotwaliwa na Urusi na ni eneo la vita kamili.

Wakati huo huo, mamlaka katika eneo la mashariki mwa Ukraine la Donetsk zimesema kuwa mji wa Pokrovsk ulishambuliwa kwa makombora ya Urusi ya masafa mafupi ya Iskander. Maafisa wamesema watu wasiopungua wanne waliuawa na wengine 34 wakiwemo watoto kujeruhiwa.